Ijue Sheria ya Fidia ya Wafanyakazi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Kutokana na uhitaji uliopo katika jamii na umuhimu wa kufahamu mambo ya sheria juu ya Fidia ya Wafanyakazi. Karibu tujifunze.

Msingi wa Sheria ya Fidia ya Wafanyakazi

Sheria hii imetungwa kwa lengo la kuhakikisha wafanyakazi wanaopata madhara wakiwa kazini au ugonjwa wakiwa kazini.  Katika maendeleo ya viwanda na sayansi shughuli zimeongezeka za kila siku na hatari pia zimeongezeka. Sheria hii imekuja kuleta fidia kutokana na kifo cha mfanyakazi au madhara aliyopata kutokana na kazi. Wafanyakazi ni kundi muhimu sana ambalo linahitaji ulinzi wa kisheria kutokana na kazi wanazofanya.

Lengo la Sheria

Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi ina malengo mbali mbali ambayo imetungwa na Bunge ili kuyakidhi. Malengo makuu  hasa;

 • Kuainisha kiwango cha madhara ya wafanyakazi na kutoa fidia stahiki kwa wafanyakazi wanaopata ajali kazini au ugonjwa kazini au kifo.
 • Kusaidia kurudisha hali ya awali ya wafanyakazi waliopata ajali kazini au ugonjwa unaotokana na kazi
 • Kuanzisha Mfuko wa Fidia kwa ajili ya wafanyakazi
 • Kuanzisha mfumo wa kusaidia kuzuia ajali na magonjwa yanayotokana na mahali pa kazi

Sheria hii ya Fidia kwa Wafanyakazi imetungwa na Bunge tangu mwaka 2008 imeanza kutumika rasmi mwishoni mwa 2015.

Matumizi ya Sheria

Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi itatumika Tanzania Bara. Haki na wajibu vilivyoanishwa katika Sheria hii itahusisha makundi yafuatayo katika matumizi yake;

 • Waajiri wote na wafanyakazi wote wa sekta binafsi na Umma
 • Kwa wafanyakazi:
 • ambao wameajiriwa katika ndege au meli za Tanzania
 • ambao wameajiriwa nje ya Tanzania lakini wamepata madhara wakiwa Tanzania na mwajiri alikuwa akiwalipa kwenye Mfuko wa Fidia kwa mujibu wa Sheria
 • wafanyakazi walioumia au kupata magonjwa kutokana na kazi zao nje ya Tanzania ikiwa Mwajiri anaendesha shughuli zake kuu ndani ya Tanzania.

Mambo Muhimu yaliyoanishiwa kwenye Sheria ya Fidia ya Wafanyakazi

Sheria hii imeainisha mambo kadhaa ya msingi ambayo mwajiri na mfanyakazi wanapaswa kuyafahamu. Mambo hayo ni kama ifuatavyo;

 1. Mfuko wa Fidia ya Wafanyakazi

Sheria imeanzisha mfuko maalum wa Fidia ya Wafanyakazi kuweza kutoa fidia kwa ugonjwa au madhara ya ajali iliyotokana na majukumu ya kazi. Mfuko huu utatoa viwango ambavyo mwajiri anapaswa kuchangia, faini endapo mwajiri atachelewa kuchangia, usajili wa waajiri wanaochangia mfuko huo. Mfuko huu ni kwa mujibu wa sheria na ni lazima kwa waajiri wote kuchangia kama ilivyo mifuko mingine ya hifadhi ya jamii mfano NSSF, LAPF, PPF, PSPF na GEPF. Hivyo waajiri wote wanapaswa kuchangia mfuko huu.

Kutokana na Kanuni za Fidia ya Wafanyakazi kuwa Serikali wa waajiri wa Taasisi za Umma watachangia kiasi cha 0.5% ya mshahara wa mfanyakazi na Mwajiri sekta binafsi atachangia kiasi cha 1% ya mshahara wa mfanyakazi.

Ikumbukuwe kiasi hiki hakipaswi kukatwa kwenye mshahara wa mfanyakazi bali ni kiwango kinachochangiwa na Mwajiri mwenyewe.

 

 1. Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia ya Wafanyakazi

Sheria hii pia imeunda Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi. Bodi ndio chombo chenye madaraka ya juu cha Mfuko wa Fidia. Bodi ya Mfuko ina uwezo wa kuingia mikataba, kununua mali za mfuko. Kazi za Bodi ni kuratibu shughuli za Mfuko, kutengeneza sera na kusimamia utekelezaji wake, kumshauri Waziri anayehusika na masuala ya Kazi.

 1. Haki ya Fidia na Ulinzi

Hili ni eneo lingine ambalo limefafanuliwa na Sheria hii ambapo imetamka bayana kuwa mfanyakazi ana haki ya kulipwa fidia pindi akipata ajali au ugonjwa. Na kwamba sheria inatamka juu ya haki ya wategemezi kupata fidia endapo mfanyakazi atafariki kutokana na sababu ya kazi yake.

 1. Madai ya Fidia

Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi imeanisha utaratibu unaotakiwa kufuatwa ili kudai fidia kwenye Mfuko wa Fidia. Zipo taratibu kadhaa za kuzingatia mfano mfanyakazi anapaswa kutoa taarifa kwa mwajiri juu ya ajali aliyopata akiwa katika majukumu ya kazi, taarifa hii inaweza kuwa ya mdomo au maandishi. Mwajiri pia anapaswa kutoa taarifa ya tukio la ajali linalomuhusu mfanyakazi wake ndani ya siku 7 tangu kupata taarifa, taarifa hii inatolewa kwenye fomu maalumu na kuwasilishwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia.

 

 1. Mchakato wa Uamuzi wa Kiasi na Aina ya Fidia

Sheria ya Fidia pia imeainisha mchakato wa kisheria wa namna ya kuhakiki endapo ugonjwa au ajali husika iliyotolewa taarifa inakidhi vigezo vya kulipwa fidia. Sheria imeweka umakini huu ili kuondoa namna zote za udanganyifu zinazoweza kujitokeza katika zoezi zima la ulipaji wa fidia.

 

 1. Fidia ya Matibabu na Ushauri

Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi imeenda mbali zaidi kwa ajili ya kutoa nafuu ya matibabu na ushauri wa kimatibabu wa wafanyakazi waliopata madhara ya ajali au ugonjwa unaotokana na majukumu ya kazi.  Mfano mfanyakazi ambaye amepata matibabu, Mfuko utakuwa unawajibika kumlipia gharama za matibabu kwa kipindi cha miaka 2 mfululizo akiwa hospitali au akiwa anapata matibabu nyumbani kwa maelekezo ya Wataalam wa Afya.

 

 1. Wajibu wa Waajiri

Ili kuondoa ukwepaji wa Waajiri kutekeleza majukumu yaliyoainishwa katika Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, sheria imeweka wajibu maalum kwa wafanyakazi. Mwajiri ana wajibu wa kutoa taarifa kuhusiana na shughuli anazofanya na juu ya wafanyakazi wake. Mwajiri anapaswa kutunza kumbu kumbu za mishahara ya wafanyakazi na endapo atahitajika kutoa nyaraka hizo kwa ukaguzi anatakiwa afanye hivyo. Endapo mwajiri atashindwa kutekeleza masharti ya wajibu wake basi anaweza kulipa faini isiyozidi Milioni 50 au kifungo kisichozidi miaka 5.

 

 1. Utatuzi wa Migogoro ya Fidia

Sheria pia imeweka utaratibu wa utatuzi wa migogoro inayotokana na ulipwaji wa fidia. Katika mchakato wa ulipaji fidia inawezekana upande wa mfanyakazi usiridhike, sheria imeweka utaratibu wa kusikiliza malalamiko ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko atafanya uamuzi na pindi akiona bado hajaridhika anaweza kukata rufaa kwa Waziri kisha Mahakama Kuu kitengo cha Ardhi.

Hitimisho

Ndugu msomaji Sheria hii ya Fidia kwa Wafanyakazi imekuja kwa wakati mwafaka kwa ajili ya kusaidia wafanyakazi wanaopata matatizo yanayotokana na kuumia kazini au kupata ugonjwa unaotokana na kazi. Ni muhimu sana kwa waajiri kutekeleza sheria hii kwani kushindwa kwako kunaweza kupelekea kifungo au faini ambayo itasababisha hasara kubwa. Pia wafanyakazi wanapaswa kuwasisitiza waajiri kuchangia mfuko huo kwa mujibu wa sheria.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

Wako

Isaack Zake, Wakili