Haki ya Usawa mbele ya Sheria

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz . Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunakwenda kujifunza juu ya Haki ya Usawa mbele ya Sheria. Jana tulijifunza juu ya Haki ya Usawa ambapo tuliona binadamu wote wanazaliwa wakiwa huru na wana usawa. bonyeza hapa kusoma   Sheria Leo.41: Haki ya Usawa. Leo tunaingia ndani kidogo kuona usawa huu mbele ya Sheria. Karibu tujifunze.

Maana ya Haki ya Usawa mbele ya Sheria

Haki ya usawa mbele ya Sheria kama tulivyoainisha kwenye makala iliyotangulia ni moja wapo ya haki za binadamu ambayo imeainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.

Hii ni haki ya msingi na haki kwa kila binadamu. Haki hii inaainishwa katika Katiba ya JMT kwenye Ibara ya 13(1) inayosema;

‘watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria’

Kwa mujibu wa Ibara hii ya Katiba ya JMT tunaona ya kwamba Katiba inawapa hadhi sawa watu wote mbele ya sheria. Hii ina maana kila mmoja wetu anawajibika sawa mbele ya sheria pasipo kujali hali, wadhifa, elimu au uchumi wa mtu.

Katiba ya JMT inaendelea kutanabaisha juu ya matumizi ya haki hii ya usawa mbele ya sheria. Kama inavyoelezwa zaidi;

  • Katiba inazuia sheria yoyote kutungwa na mamlaka yoyote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwekwa sharti lolote la ubaguzi ama dhahiri au kwa taathira yake
  • Katiba inatamka bayana juu ya haki za raia, wajibu na maslahi ya kila mtu na jumuiya ya watu yatalindwa na kuamuliwa na mahakama na vyombo vinginevyo vya mamlaka ya Nchi vilivyowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria
  • Kwamba ni marufuku kwa mtu yeyote kubaguliwa na mtu au mamlaka yoyote inayotekeleza madaraka yake chini ya sheria yoyote au katika utekelezaji wa kazi au shughuli yoyote ya mamlaka ya Nchi.

Hii ni kwa mujibu wa Ibara ya 13 (2),(3),(4) ya Katiba ya JMT.

Katiba ya JMT pia imaainisha tafsiri ya neno ubaguzi ili kuondoa tashwishi ambayo inaweza kusababishwa na neno hili kutokueleweka au kutumiwa vibaya kwa mujibu wa Ibara ya 13 (5) likimaanisha;

Ubaguzi; lina maana ya kutimiza haja au mahitaji mengineyo kwa watu mbalimbali kwa kuzingatia  utaifa wao, kabila, pahala walipotokea, maoni ya kisiasa, rangi, dini, jinsia, au hali yao ya maisha kwa namna mbayo watu wa aina fulani wanafanywa au kuhesabiwa kuwa dhaifu au duni na kuwekewa vikwazo au masharti ya vipingamizi ambapo watu wa aina nyingine wanatendewa tofauti au wanapewa fursa au faida iliyoko nje ya masharti au sifa za lazima.

Hata hivyo neno ubaguzi halitafafanuliwa kwa namna ambayo itazuia Serikali kuchukua hatua za makusudi zenye lengo la kurekebisha matatizo mahsusi katika jamii.

Namna Katiba inavyohakikisha Usawa mbele ya Sheria

Ibara ya 13 (6) ya Katiba ya JMT inaonesha namna ambavyo dhumuni la kuhakikisha usawa wa watu wote mbele ya sheria.

  • Mtu atakuwa na haki ya kusikilizwa kikamilifu wakati jambo linalohusu haki na wajibu wake lipo mbele vya vyombo vya maamuzi. Pia ana haki ya kukata rufaa au kupata nafuu nyingine ya kisheria kutokana na maamuzi ya mahakama au chombo hicho kinginecho kinachohusika.
  • Ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo.
  • Ni marufuku kwa mtu yeyote kuadhibiwa kwa sababu ya kitendo chochote ambacho alipokitenda hakikuwa ni kosa chini ya sheria, na pia kwamba ni marufuku kwa adhabu kutolewa ambayo ni kubwa kuliko adhabu iliyokuwapo wakati kosa linalohusika lilipotendwa
  • Katika shughuli zote za upelelezi na uendeshaji wa mambo ya jinai na katika shughuli zote ambapo mtu anakuwa chini ya ulinzi bila uhuru au katika kuhakikisha utekelezaji wa adhabu heshima ya mtu itatunzwa kwa ajili ya kuhifadhi haki na usawa wa binadamu.
  • Ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha.

Hitimisho

Usawa mbele ya sheria ni haki ya msingi kwa kila mwananchi kama tulivyowahi kuchambua kuwa sheria inawahusu watu wote kwenye eneo husika. Hivyo ni lazima vyombo vinavyohusika na usimamizi na utekelezaji wa sheria kuchukua hatua zinazostahili kutekeleza kila jambo kwa mujibu wa sheria na kuwatendea watu wote pasipo kuwabagua kwa namna yoyote ile ili taifa liweze kusimamia haki na kustawi katika nyanja zote yaani kiuchumi, kisiasa, kijamii na kidini.

 

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Wako

Isaack Zake, Wakili