Utaratibu wa Umiliki wa Ardhi kwa njia ya Serikali

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tuliangalia juu ya njia ya Zawadi. Leo tunaendelea na mfululizo wa uchambuzi wa njia ya Serikali. Karibu tujifunze.

Umiliki wa Ardhi kwa njia ya Serikali

Kama tunavyofahamu kuwa ardhi yote ni mali ya umma na Rais ni mdhamini wa ardhi husika. Katika mfumo wa utawala wa ardhi Rais anakaimisha majukumu ya ardhi kwa Waziri mwenye dhamana ya ardhi na Makamishna wa ardhi katika kila eneo la nchi.

Katika njia ambazo tumejadili za umiliki wa ardhi, pia umiliki kwa kupewa na Serikali ni mojawapo ya njia za umiliki yenye uhalali kwa mtu. Katika makala hii tunakwenda kuangalia utaratibu sahihi wa kumiliki ardhi au eneo kwa kupata nyaraka za kiserikali.

Aina za mchakato wa umiliki wa ardhi kwa njia ya Serikali

  • Mchakato unaoanzishwa na Serikali; hapa serikali inachukua jukumu la awali la kutafuata maeneo na kufanya upimaji wa viwanja kisha kualika wananchi wenye nia ya kupata umiliki kufanya maombi na baadae kupewa hati za umiliki.
  • Mchakato unaoanzishwa na mwananchi au wananchi; hapa wananchi wenyewe au mwananchi anakuwa na eneo lake ambalo anaweza kuwa amelipata kimila au kwa zawadi au kwa urithi ambapo anaamua kufanya upimaji ili kupata hati za umiliki.
  • Mchakato unaoanzishwa na taasisi; hapa taasisi mbalimbali ikiwa za umma au binafsi zinachukua hatua za kutafuta maeneo na kufanya uwekezaji kwa njia ya kupima na kuuza viwanja vyenye hati za umiliki kwa wananchi.

 Utaratibu wa umiliki ardhi kwa njia ya Serikali

Katika ugawaji wa ardhi kama zawadi upo utaratibu ambao unapaswa kuzingatiwa ili uhalali wa zawadi hiyo ya ardhi ubainike. Ardhi haitolewi tu kiholela bali kuna misingi ya utoaji na taratibu za kuzingati.

Ufuatao ni utaratibu wa kutoa ardhi kwa Serikali;-

  1. Uwepo wa ardhi

Hili ni jambo la msingi sana katika umiliki wa ardhi kupitia serikali. Ardhi ndio msingi wa umiliki pasipo ardhi ya kumiliki serikali haiwezi kukupa eneo. Katika mgawanyo wa ardhi kwa mujibu wa sheria ya ardhi kuna ardhi ya hifadhi, ardhi ya kijiji na ardhi ya jumla. Serikali inaweza kutoa umiliki katika ardhi ya jumla. Ardhi ya kijiji una utaratibu wake wa jinsi ya kutolewa kwa wananchi kwa umiliki tofauti na ardhi ya jumla.

  1. Upimaji wa maeneo kwa madhumuni mbalimbali

Hatua muhimu ya msingi katika kupatiwa eneo la umiliki na Serikali ni upimaji na ramani. Serikali inafanya mchakato wa kutengeneza ramani ya mipango miji na kupima viwanja au maeneo kwa shughuli mbalimbali. Hapa ardhi inapangwa kwa matumizi mbalimbali ikiwa ni maeneo kwa ajili ya biashara au makazi au viwanda n.k

  1. Maombi maalum ya umilikishwaji wa eneo

Mwananchi au wadau baada ya umimaji wanaalikwa kufanya maombi maalum katika mamlaka ambazo viwanja au maeneo hayo inahusika. Viwanja vinaweza kuwa chini ya Manispaa au Halimashauri za miji ambapo wenye mahitaji wanaweza kupeleka maombi yao na kufanyiwa kazi kwa mujibu wa taratibu za umilikishaji wa ardhi.

  1. Kusajiliwa kwa hati za umiliki wa eneo

Endapo maombi ya mwananchi yamekubaliwa basi mamlaka husika itaandaa hati ya umiliki wa eneo kulingana na masharti ya matumizi na muda ambao mtu anaweza kumiliki ardhi husika. Hati hizi zinaandaliwa kwa majina ya mmiliki na anawajibika kufuata masharti yote sawa na kusudio la eneo alilopewa na mamlaka. Hati hizi zina muda wa kuanzia miaka 33 au 66 au 99.

Hitimisho

Sheria ya ardhi inatambua juu ya kumilikishwa kwa wananchi maeneo au ardhi kupitia mchakato wa usajili wa hati za ardhi kwa mamlaka husika. Ni lengo la serikali kuhakikisha maeneo yote ambayo yana shughuli za kibinadamu ikiwa ni makazi au viwanda au biashara basi pawe na hati za umiliki ili kuiwezesha kupata kodi ya ardhi na majengo kutoka kwa wamiliki. Ni muhimu kila mwananchi mwenye eneo kuhakikisha anaanzisha mchakato wa upimaji wa eneo kwani utaongeza thamani ya eneo na uhakika wa ulinzi endapo eneo husika mamlaka za serikali zimehusika katika mchakato wa upatikanaji wake.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili