Utaratibu wa Umiliki wa Ardhi kwa njia ya Kusafisha Eneo

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tuliangalia juu ya njia ya Serikali kwa kupewa Hati ya Umiliki wa ardhi. Leo tunaendelea na mfululizo wa uchambuzi wa njia ya Kusafisha Eneo. Karibu tujifunze.

Umiliki wa Ardhi kwa Kusafisha Eneo

Mojawapo ya zawadi ambazo taifa hili limejaliwa ni uwepo wa ardhi ya kutosha. Tanzania ndio nchi kubwa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Ardhi yote kama tunavyofahamu ipo chini ya usimamizi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama mdhamini wa mali hii ya umma. Pamoja na nafasi ya Rais kama mdhamini wa ardhi yote ya nchi, wananchi ndio wanakuwa na matumizi mbalimbali ya ardhi husika.

Kwa ukubwa wa ardhi iliyopo katika Tanzania, yapo maeneo ambayo hayamilikiwi na mtu mmoja mmoja au jamii au kijiji yanahesabika kama mapori au vichaka.

Umiliki tunaouzungumzia hapa ni ule mtu anaweza kwenda kwenye eneo ambalo halipo chini ya umiliki wa mtu au kijiji au familia au ukoo yaani ni kichaka au pori tu.

 

Utaratibu wa umiliki ardhi kwa njia ya Kusafisha Eneo

Katika utaratibu wa umiliki kwa njia ya kusafisha eneo au pori yapo mazingira ambayo yanaweza kumsaidia mtu kuhalalisha umiliki wa maeneo husika.

Ufuatao ni utaratibu wa kupata ardhi kwa kusafisha eneo;-

  1. Uwepo wa ardhi

Hii ni hatua ya kwanza na muhimu kwa kudhibitisha juu ya kumiliki eneo kwa njia ya kusafisha eneo au kichaka/pori. Ni lazima liwepo eneo ambalo si mali ya mtu au kijiji au ukoo. Zipo familia au koo nyingi zimekuwa zikipata maeneo yao ya kiasili kwa njia hii yaani wanahamie eneo fulani na kusafisha kwa ajili ya kufanya shughuli za uzalishaji. Kigezo ambacho kina umuhimu sana ili kumiliki kwa njia ya kusafisha eneo ni eneo husika kutokuwa chini ya umiliki wa mtu au watu.

  1. Kusafisha eneo

Hatua hii ya pili ni muhimu sana kwani msingi wa uhalali wa umiliki ni hatua ulizochukua kuhusiana na eneo husika. Mtu anapata uhalali kwa kuchukua hatua za kusafisha eneo husika endapo ni pori au kichaka kikubwa. Mtu anamiliki kwa kiwango kile ambacho amechukua hatua ya kusafisha, eneo ambalo limesafishwa ndilo linahesabika kama mali ya mtu aliyechukua hatua hiyo. Wengi wanachukua hatua ya kulima mkuza yaani ufyekaji wa eneo kuaisha mipata ya umiliki.

  1. Kufanya shughuli za uzalishaji au makazi

Mtu anayetaka kufahamika kama mmiliki halali wa eneo ambalo amechukua hatua za kusafisha au kuondoa pori ni lazima aoneshe shughuli anazofanya katika hilo eneo ikiwa ni shughuli za kilimo au kufuga. Pia mtu anaweza kuanzisha makazi katika eneo husika hii itaendelea kumpa uhalali kijamii na kisheria kuwa eneo hilo ni milki yake.

  1. Kuwepo katika eneo kwa muda mrefu

Hii pia ni moja ya sababu ambayo inampa mtu uhalali wa kumiliki eneo kwa njia ya kusafisha kichaka au pori. Ni lazima mhusika aoneshe kuwa anakaa au anafanya shughuli zake katika eneo hilo kwa muda mrefu. Muda mrefu kutokana na masuala ya ardhi ni kipindi cha walau miaka 12 mfululizo katika eneo.

Hitimisho

Njia ya kusafisha maeneo na kumiliki imekuwa ni njia ya umiliki tangu zamani na familia au koo nyingi zimepata umiliki huo wa maeneo na kuendelea kuyamiliki hata sasa. Hatahivyo, kumiliki kwa njia hii maeneo ya mjini si rahisi kwani maeneo karibu yote yanamilikiwa na si rahisi kukuta pori au kichaka maeneo ya miji pasipo kuwa na umiliki wa mtu au kuwa eneo la hifadhi. Muhimu kwa mtu aliyepata umiliki kwa njia ya kusafisha eneo kufanya taratibu za kisheria kulingana na eneo alilopo ikiwa ni serikali ya kijiji cha karibu au mamlaka husika ili atambulike kuwa ni mmiliki wa eneo husika.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili