Nini Kifanyike endapo mtu atafariki pasipo wosia?
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunaendelea kujifunza mambo kadhaa ya umuhimu katika sheria za mirathi. Karibu tujifunze kwa pamoja.
Msingi wa somo la leo
Mara kwa mara linapoibuka suala la kifo wanadamu wanaingiwa na hofu kuu kwa kujua au kutokujua. Masuala ya mirathi na wosia ni mojawapo ya maeneo ambayo watu wengi hawapendi kujifunza au kuyasikia lakini hayana budi kutokea katika mfumo wa maisha yetu ya kila siku.
Tangu enzi na enzi mambo ambayo yanaleta ugomvi na hata kusababisha misiba mingine ni hali ya kutokujiandaa kwa marehemu na wanafamilia wanaobaki kuhusiana na mgawanyo wa mali na mwendelezo wa matakwa ya marehemu mara baada ya kifo chake.
Sisi sote tumekuwa mashahidi wa mizozo au tumehusika kwa njia moja ama nyingine katika mizozo ya muda mrefu juu ya mali za marehemu. Hali hii imechangia jamii kukwama kwa muda mrefu na kuishia mahakamani mara kwa mara na hatimaye amani kutoweka na undugu kuingia mashakani.
Hivyo katika makala hii tunaenda kujifunza mojawapo ya eneo linalosabaisha kuibuka kwa migogoro ya mirathi na hatua stahiki zinazopaswa kuchukuliwa kwa wahusika.
Maana ya Wosia
Kama tulivyowahi kuzungumza kwenye makala zilizopita juu ya wosia, ni tamko au matamshi ya mtu kabla hajafariki yakielezea namna mali yake itakavyoshughulikiwa/itakavyomilikiwa baada ya kifo chake.
Wosia inaweza pia kutafsiriwa kama maelezo ya marehemu yam domo au maandishi kabla ya kifo chake juu ya maziko yake yatakavyokuwa, juu ya mali zake jinsi zitakavyorithishwa na maelekezo mengine kwa wanafamilia wake
Kwa mtu ambaye anafariki huku ameacha wosia na kumteua mtekeleza wosia, changamoto za mirathi kama zipo ni chache sana kwani kinachofuatwa ni matakwa ya marehemu aliyoandika au kutamka katika wosia.
Hatahivyo, changamoto inajitokeza pale ambapo marehemu anafariki pasipo kuandika wosia. Kama tunavyofahamu kuwa kila binadamu kama tusivyoijua siku ya kuzaliwa kadhalika hatuijui siku ya kufariki kwetu. Wengi wanakutwa na mauti wakiwa hawajaandika wosia na hivyo kufariki huku wakiacha maswali mengi kwa warithi wao juu ya hatma zao na mambo mengine.
Leo tunaangalia hatua za msingi ambazo wanafamilia wanapaswa kuzingatia katika kushughulikia mirathi iliyoachwa pasipo wosia.
- Kufanya kikao cha familia
Mara baada ya kutokea kifo cha marehemu ambaye anaacha familia na mali kadhaa ambazo zinahitaji usimamizi wa mirathi ni muhimu sana wanafamilia wa karibu kukutana maramoja wakati wa msiba na kuanza kuandaa taratibu husika. Hapa inazungumzia wanafamilia wa karibu ikiwa kifo ni cha baba basi mke na watoto na ndugu wa karibu waweze kukutana na kuweka mkakati namna ya kushughulikia suala la msiba. Kipaombele cha kikao hiki ni kuona namna marehemu anavyoweza kuzikwa na wakubaliane eneo la kuzika. Hii ni muhimu kwani changamoto nyingi za mirathi zinaanza na ndugu kugombea maiti. Ni vyema tukafahamu hata kwa namna gani tunavyoweza kugombea mwili wa marehemu bado hatoweza kurudi kwetu na ile kupata haki ya marehemu kuzikwa kule ambapo unadhani angetaka hakumpatii mtu haki au kumnyima mwengine haki katika kudai mirathi kwa marehemu. Ni muhimu ndugu wa karibu kuchukua wajibu na kutoa maamuzi ya pamoja katika suala hili.
- Kufanya maziko ya marehemu
Jambo la msingi ni kuhakikisha mwili mwa marehemu unapumzishwa kulingana na taratibu ambazo jamii husika au marehemu amekuwa akiamini. Katika eneo hili pia tunashuhudia mizozo mingi kati ya ndugu pale wanapojikuta kila upande ungetaka marehemu azikwe kwa taratibu zao. Ni vyema tukafahamu kuwa sisi tuliobaki tunao wajibu wa kutekeleza wa kuhakikisha marehemu anazikwa kwa heshima zote pasipo mvutano, hii itatujengea mshikamano na heshima miongoni mwa jamii zetu kwani aina ya maziko haiwezi kumbadili marehemu kuwa wa imani nyingine.
- Kufanya kikao cha wanafamilia wa pande zote
Kikao hiki kitahusika hasa na hatma ya mali za marehemu pamoja na kutambua warithi wake halali. Ni vyema viongozi wa familia kufanya kikao hiki mara baada ya mazishi ili kuepuka hali ya kutoelewana endapo baadhi ya ndugu watakuwa na tofauti za kimtazamo. Katika kikao hiki agenda kuu ni kutambua warithi halali wa marehemu na mali za marehemu pamoja na madeni kama yapo. Katika kikao hiki ndipo migogoro mingi inaibuka iwapo marehemu alikuwa na mali, wanaanza kujitokeza watu ambao kwa kawaida hawakufahamika. Busara ya wazee na viongozi wa familia inapaswa kutumika kuhakikisha warithi halali wanapata haki zao. Ni muhimu sana kuzingati, unakuta wakati wa msiba ndipo warithi wengine wanaanza kujitokeza, je, walikuwa wapi siku zote kabla ya kifo? Kama marehemu mwenyewe hakutaka kuwatambulisha akiwa hai, je angetaka kuwatambulisha sasa akiwa amekufa? Haya ni mambo yanayohitaji hekima na busara katika kuyatatua.
Hitimisho
Leo tumeangalia hatua za awali katika kushughulikia mirathi ya mtu aliyefariki pasipo wosia. Ni muhimu sana kwa mtu kuacha wosia ili kuepusha familia yako na madhara yanayoweza kujitokeza pindi utakapofariki na kuwaachia migogoro isiyoisha na kupoteza muda mwingi wa uzalishaji.
‘Andika wosia sasa, maadam unaishi leo’
Katika makala inayofuata, tutaendelea na hatua za msingi za kuchukua katika kushughulikia mirathi isiyo na wosia.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.
Muhimu
Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .
‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’
Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.
Wako
Isaack Zake, Wakili