Nini Kifanyike endapo mtu atafariki pasipo wosia?

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu  kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunaendelea kujifunza na mfululizo wa makala ambayo tulianza hapo. Karibu tujifunze kwa pamoja.

Hatua za kuchukua katika mirathi ya mtu asiye na wosia

Katika makala iliyotangulia tuliweza kuangalia hatua muhimu za kuchukua katika kushughulikia mirathi ya mtu aliyekufa pasipo wosia. Hatua hizo tulizoangalia ni;-

  1. Kufanya kikao cha familia
  2. Kufanya maziko ya marehemu
  3. Kufanya kikao cha wanafamilia wa pande zote

Leo tunaendelea katika kuchambua hatua nyingine za muhimu na kuzingatia ili kushughulikia mirathi ya mtu asiye na wosia.

  1. Kuteua msimamizi au wasimamizi wa mirathi

Hii ni hatua muhimu katika kushughulikia mirathi isiyo na wosia. Sheria inaongoza kuwa msimamizi wa mirathi atateuliwa na wanafamilia au wanaukoo wa marehemu. Ni muhimu sana kwa wanafamilia katika suala la uteuzi wa msimamizi wa mirathi kuwa makini kwani changamoto nyingine zinaibuliwa na wasimamizi wa mirathi kwa kutokuwa waaminifu. Ni vyema msimamizi wa mirathi akawa mtu mwaminifu anayeweza kusimamia kikamilifu mali ya marehemu. Familia inaweza kumteua msimamizi wa mirathi akiwa ni miongoni mwa warithi au asiye mrithi. Pia anaweza kuwa msimamizi mmoja au wawili kutegemea makubaliano ya familia husika. Katika uteuzi wa msimamizi wa mirathi ni vyema pande zote za familia zikashirikishwa ili kuondoa uwezekano wa mgongano baina ya wanafamilia.

 

  1. Wasimamizi kufungua shauri la mirathi

Hatua ya muhimu zaidi ni kwa msimamizi au wasimamizi wa mirathi kufungua shauri la mirathi katika mahakama husika. Mashauri ya mirathi husikilizwa kwenye mahakama za Mwanzo au Mahakama Kuu. Wasimamizi wanapaswa kukamilisha taratibu zote za maziko na kuorodhesha warithi halali wa marehemu. Endapo katika mchakato huu kutajitokeza mapingamizi basi ni jukumu la mahakama kuamua masuala hayo. Baada ya shauri la mirathi kufunguliwa, Mahakama itampatia msimamizi au wasimamizi hati za usimamizi wa mirathi ili waweze kutambulika katika taasisi mbalimbali katika mchakato wa kukusanya mali na madeni ya marehemu.

 

  1. Wasimamizi kutimiza wajibu wao kwa haki

Ni kazi ya msimamizi au wasimamizi wa mirathi ya marehemu asiye na wosia kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria. Wajibu mkuu wa msimamizi ni kukusanya madeni na mali za marehemu na kuhakikisha madeni yanalipwa kwa wadeni halali na kiasi cha mali zilizobaki kinagawiwa kwa warithi wa marehemu. Pamekuwa na changamoto kubwa kwa baadhi ya wasimamizi kwa kutokujua wajibu wao au kwa makusudi wanageuka kuwa wamiliki wa mali husika na kutokamilisha zoezi la ugawaji wa mali za marehemu kwa warithi. Hii inaibua mgogoro mkubwa miongoni mwa jamii na kuwakosesha warithi haki zao. Muhimu kwa msimamizi kutimiza wajibu wake ndani ya muda usiozidi miezi 6 na kutoa taarifa Mahakamani ili shauri husika liweze kufungwa.

Hitimisho

Ni muhimu sana kwa familia na wanaukoo kuzingatia mwongozo wa hatua hizi ambazo tumeziangalia tangu makala iliyopita. Muhimu zaidi kwa mtu kuandika wosia ili kusaidia kuepuka matatizo na migogoro inayojitokeza mara baada ya kifo kutokea katika familia. Muhimu zaidi kwa mtu kutambulisha watoto au ndugu muhimu na maeneo ambayo anamiliki ili iwe kazi rahisi kwa msimamizi wa mirathi kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.

‘Andika wosia sasa, maadam unaishi leo’

Katika makala inayofuata, tutaendelea na hatua za msingi za kuchukua katika kushughulikia mirathi isiyo na wosia.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili