Zipi sifa za Msimamizi wa Mirathi?

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunaendelea kujifunza na mfululizo wa makala zinazohusu masuala ya mirathi. Karibu tujifunze kwa pamoja.

Msimamizi wa Mirathi

Msimamizi wa mirathi ni mtu ambaye anateuliwa na familia na kudhibitishwa na mahakama kusimamia mirathi ya marehemu ambaye alifariki pasipo wosia.

Msimamizi wa mirathi anateuliwa pale ambapo marehemu alifariki pasipo kuacha wosia. Endapo marehemu atafariki akiwa ameacha wosia basi atateuliwa Mtekeleza wosia ambaye anakuwa ametajwa na marehemu ndani ya wosia na si msimamizi wa wosia.

Msimamizi wa mirathi ni mtu muhimu sana katika suala zima la mirathi yaani mali zote za marehemu pamoja na madeni yake jinsi ambayo yanapaswa kushughulikiwa. Kwa kuwa jukumu la usimamizi wa mirathi ni jukumu zito ambalo linabeba hatma ya warithi na kuhusika na mali za marehemu, jukumu hili linapaswa kukabidhiwa kwa mtu makini mwenye uwezo wa kutekeleza pasipo upendeleo wala kupotosha haki za warithi.

Sifa za msimamizi wa Mirathi

Watu wengi wanateuliwa kuwa wasimamizi wa mirathi pasipo kuangalia mambo au vigezo muhimu vya kuzingatia. Unaweza kukuta katika familia anateuliwa mtu mkubwa kiumri au kulingana na jinsia yake. Pamoja mambo hayo ni muhimu lakini si vigezo vinavyoweza kusaidia kutimiza wajibu wa usimamizi wa mirathi.

Zifuatazo ni baadhi ya sifa za msimamizi wa mirathi;-

  1. Msimamizi wa mirathi awe mtu wa busara, hekima na mvumilivu

Katika mchakato wa kufuatilia haki za marehemu na kuhakikisha warithi wanapata stahiki zao ni lazima kuwa na msimamizi ambaye anaongozwa na busara, hekima na uvumilivu. Sote tunafahamu kifo kinapojitokeza katika familia ambapo hakuna wosia basi kila mmoja anakuwa katika hamaki kutaka kujua hatma ya stahiki zake. Katika mazingira haya ni rahisi sana kujitokeza hali ya kutokuelewana. Jambo la msingi kwa familia na ukoo unapaswa kuchagua mtu au watu ambao wana tabia zinazoshabihiana na uvumilivu na hekima. Endapo msimamizi atakuwa mtu wa vurugu ni vigumu shauri la mirathi kumalizika salama.

  1. Msimamizi awe mtu mwaminifu

Uaminifu ni kigezo muhimu sana katika kutekeleza wajibu wa usimamizi wa mirathi. Msimamizi wa mirathi anakuwa amesimama kwenye nafasi ya marehemu, huu ni wajibu mkubwa unahitaji hofu ya Mungu kuhakikisha kila anayehusika anapatiwa haki yake kikamilifu. Siku za karibuni pamekuwa na changamoto ya uaminifu katika utekelezaji wa majukumu ya usimamizi wa mirathi kwani wasimamizi wengi wanajigeuza kuwa wamiliki wa mali na kuzifuja mali au kuhamisha au kuuza kwa manufaa yao pasipo kuangalia maslahi ya warithi husika. Hivyo familia au ukoo wakati wa kumteua msimamizi ni muhimu sana kuangalia kigezo cha uaminifu kwa mtu anayeteuliwa.

  1. Msimamizi awe na sifa ya uongozi

Sifa ya uongozi katika zoezi zima la usimamizi wa mirathi ni muhumu sana. Kama tunavyofahamu familia inapokubwa na msiba, taharuki ni lazima itaibuka kwa wanafamilia. Msimamizi wa mirathi ndiye mtu pekee anayeweza kutoa dira njema kwa familia na mwelekeo endapo patatokea mgongano baina ya wanafamilia. Uongozi ni kuonesha njia kwa vitendo, msimamizi ni lazima awe mtu wa msimamo na mwenye kauli dhabiti asiyeyumbishwa katika maamuzi yake kutegemea na upande wa wanafamilia. Kama tujuavyo familia zetu za kiafrika nyingi ni zile ambazo.

  1. Msimamizi wa mirathi awe na elimu

Katika nyakati ambazo tunaishi sasa kigezo cha elimu ni cha msingi sana katika kushughulikia masuala mbalimbali ikiwepo suala la mirathi. Watu wengi wanadhani masuala haya yanahitaji kuwa mtu mwenye umri mkubwa tu la hasha elimu pia itasaidia kwa msimamizi kuweza kujua namna sahihi ya kutekeleza wajibu wake. Elimu hii inayosemwa hapa walau msimamizi awe na uwezo wa kusoma na kuandika ikibidi katika lugha ya Kiswahili na kiingereza. Hii haimaanishi kuwa msimamizi mwenye elimu ndiye atakuwa sahihi bado kuna vigezo vingine ambavyo familia inapaswa kuzingatia. Pia pamekuwepo na wasimamizi walio na elimu nzuri na wakaaminiwa na warithi lakini wakatumia elimu yao kupotosha haki ya warithi.

  1. Msimamizi awe mpenda haki

Katika usimamizi wa mirathi suala zima linahusisha upatikanaji wa haki za warithi halali na wadai wa marehemu. Msimamizi ni lazima awe mpenda haki yaani mtu asiyetaka kujihusisha na dhuluma kwa namna yoyote akitaka kuwapendelea wadai au warithi. Kazi ya msimamizi ni kama ile ya hakimu mahakamani inapofika katika ugawaji wa mali ya marehemu. Msimamizi ahakikishe warithi halali wa marehemu wanapata haki yao kikamilifu pasipo ubaguzi wa aina yoyote.

Hitimisho

Kama tulivyoweza kuzitazama sifa muhimu za msimamizi wa mirathi ambazo familia zinapaswa kuziangalia kabla ya kuteua msimamizi wa mirathi. Tunafahamu endapo marehemu ameacha fedha na mali wapo wengi watakaotaka kujitokeza kusimamia mirathi lakini ni wachache wenye vigezo vya kuwafaa warithi. Warithi wanayo haki na wajibu wa kuhakikisha msimamizi wa mirathi anayeteuliwa ni mtu anayeshuhudiwa na sifa husika na nyingine ambazo ni njema.

‘Andika wosia sasa, maadam unaishi leo’

Katika makala inayofuata, tutaendelea na hatua za msingi za kuchukua katika kushughulikia mirathi isiyo na wosia.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili