25. Usitishaji wa Ajira kwa sababu ya Uwezo mdogo wa Kazi
Utangulizi
Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala za hivi karibuni tumekuwa tukichambua sababu na taratibu mbalimbali zinazoweza kusababisha au kufuatwa ili kusitisha ajira ya mfanyakazi kihalali.Leo tunaendelea kuangalia juu ya usitishaji wa Ajira kwa sababu ya uwezo mdogo wa kazi.
Maana ya Uwezo Mdogo wa Kazi
Uwezo mdogo wa kazi ina maana utendaji wa mfanyakazi kutokidhi viwango au vigezo vilivyowekwa katika kutimiza majukumu yake ya kazi. Katika sehemu za kazi kuna mwongozo wa kazi ambapo mfanyakazi anapaswa kuzingatia na kufuata ili kutimiza majukumu yake. Mwongozo wa kazi unaainisha majukumu, namna ya utekelezaji na viwango vinavyopaswa kufikiwa na mfanyakazi ili kukamilisha kazi husika.
Katika mahusiano ya ajira baina ya mfanyakazi na mwajiri kunaweza kujitokeza hali ya mfanyakazi kutokidhi viwango vya kazi kwa kutokutekeleza majukumu yake ipasavyo. Iwapo itathibitika kuwa mfanyakazi anaonesha uwezo mdogo wa kazi basi inaweza kuwa sababu mojawapo ya kusitisha ajira ya mfanyakazi.
Sababu zinazoweza kuchangia uwezo mdogo wa kazi
Sheria ya Ajira inaanisha aina za sababu zinazoweza kuchangia mfanyakazi kuonesha uwezo mdogo kazini ni pamoja na;
- Utendaji usioridhisha
Hali ya utendaji usioridhisha inawezekana kusababishwa na mfanyakazi mwenyewe kwa kuwa mzembe asiyezingatia vigezo vya kazi aliyopewa. Mwajiri anawajibika kuweka vigezo maalum vya utendaji wa kazi mahali pa kazi. Vigezo husika ni lazima vifahamike na mfanyakazi.
- Kuumia
Yapo mazingira ambayo mfanyakazi anaweza kuumia kazini au mahali pengine na kusababisha uwezo wake wa kutimiza majukumu kupungua siku kwa siku. Hivyo ni muhimu kwa mwajiri kuangalia namna ya kuwezesha mfanyakazi husika kuachishwa kazi endapo kuumia huko kunaathiri kwa kiwango kikubwa shughuli za mwajiri.
- Ugonjwa
Mfanyakazi anaweza kupatwa na maradhi ambayo yanaweza kusababisha utendeji wake na uwezo wa kutimiza majukumu kupungua. Sababu ya ugonjwa inaweza kutumika katika kusitisha ajira kutokana na uwezo mdogo mahali pa kazi.
Katika mfululizo wa kuchambua sababu hizi zinazochangia uwezo mdogo mahali pa kazi tutakwenda kuziangalia sababu moja baada ya nyingine na utaratibu mwafaka wa kisheria ili sababu husika ziweze kuwa za haki na halali kwa mujibu wa sheria.
Hitimisho
Ni muhimu kwa mfanyakazi na mwajiri kufahamu kuwa uwezo mdogo mahali pa kazi unaweza kusababisha mahusiano ya kiajira baina yao kusitishwa. Hatahivyo, mwajiri hana mamlaka ya moja kwa moja kusitisha ajira pasipo kuzingatia taratibu za kisheria kama zinavyotambuliwa na kanuni za utendaji bora mahala pa kazi.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.
Muhimu
Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .
‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’
Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.
Wako
Isaack Zake, Wakili.