Kwa Nini ni Muhimu kwako Kufahamu masuala ya Mirathi?

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunaendelea kujifunza na mfululizo wa makala zinazohusu masuala ya mirathi. Karibu tujifunze kwa pamoja.

Maana Mirathi

Mirathi ni jumla ya mali na madai au madeni aliyoacha marehemu ambayo ana haki nayo au anawajibika kulipa. Kama tunavyofahamu kuwa wanadamu wote tunaishi kwa kitambo tu hivyo mali na madeni ambayo tunatengeneza ipo siku tutaviacha hapa duniani.

Katika makala hii ya leo tunakwenda kuangalia sababu za msingi ambazo zinakulazimu kuchukulia umuhimu mkubwa maswala haya ya mirathi katika maisha yako ya kila siku.

Zipo sababu nyingi ambazo zinakupasa kuweka umuhimu katika maswala ya mirathi, hata hivyo hapa tutajadili baadhi ya sababu.

  1. Maisha yako au ya watu wako wa karibu ni ya muda

Ni muhimu sana ndugu yangu kuwa na ufahamu kuwa maisha yetu yana muda yaani tunazaliwa, tunaishi na kisha kufa. Katika safari zetu za maisha kama vile hatukuwa na ufahamu kuwa tunazaliwa lini vivyo hivyo hatujui tutakufa lini au ndugu zetu wa karibu wataondoka lini. Kufahamu mambo ya mirathi na kuanza kujiandaa mapema kutasaidia watu kuacha mazingira mazuri katika familia na jamii zao kwa ujumla. Ndugu yangu ukifahamu ukweli huu utakusaidia wewe kujiandaa au kuwaandaa ndugu au wazazi wako ili mambo haya yasilete mgongano mara baada ya mauti kukufika au kuwafika watu wa karibu.

  1. Migogoro ya kifamilia

Masuala ya mirathi ni eneo mojawapo la sheria ambalo lina migogoro mingi ikiwa ni mahakamani au kwenye jamii kwa ujumla. Tumeona familia zikivunjika kwa kifo cha baba au mama au ndugu aliye nguzo kwenye familia. Tumeshuhudia wajane wakidhulumiwa, na yatima wakiingia kwenye matatizo makubwa kutokana na vifo vya wazazi. Ufahamu na kuchukua hatua stahiki juu ya maandalizi ya mirathi kutaepusha familia na ndugu zako kuingia kwenye migogoro. Ipo dhana kwa watu wengi kutokuchukua hatua wakidhani kuwa hata wao wakiondoka ndugu wataendelea kukaa kwa amani, jambo hili si la kweli maana tumeshuhudia ndugu wa kuzaliwa wakiuana kwa sababu ya mirathi. Chukua hatua mapema kuokoa familia yako.

  1. Mwingiliano wa kijamii na kidini

Kama tunavyofahamu jamii yetu ya Tanzania imekuwa na mwingiliano mkubwa wa kikabila na kidini yaani watu wanaona wakiwa na dini tofauti na makabila tofauti. Mwingiliano huu wa jamii unaibua changamoto kubwa endapo mmoja wapo atafariki na kuanza kujiuliza juu ya mila zipi zitatumika au sheria za dini ipi zitatumika. Iwapo wewe ndugu yangu ukachukua tahadhari mapema kwa kupata ushauri kwa wataalam wa sheria itakusaidia sana kuepusha mgongano ndani ya familia kwenye tofauti hizi za dini na hata makabila.

  1. Mwongozo wa Katiba

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatoa maelekezo juu ya kila mmoja kuwa na haki ya kumiliki mali pasipo kujali mahali anapotoka au jinsia yake. Hii imetokana na mabadiliko ya Katiba yaliyofanyika mwaka 1984. Tunafahamu kundi la wanawake wamekuwa wakinyanyaswa kwa muda mrefu kuhusiana na mambo ya mali. Hivyo kama mtanzania unapaswa kufahamu pia wanawake wanayo haki ya kurithi na hata kurithisha mali zao walizopata binafsi au wakiwa kwenye ndoa.

  1. Tamaa za mali na dhuluma

Hali ya mabadiliko katika mwenendo wa watu kwenye jamii imeamsha tabia ya kutokuwa na upendo. Watu wamekuwa na tamaa za mali na kupenda kudhulumu. Misiba ya watu waliokuwa na mali inagubikwa na vurugu nyingi za watu kutaka kupigania mali za marehemu na kuwaacha warithi halali wakihangaika kwa kukosekana maandalizi ya awali. Kuepusha watu wasio na haki juu ya mirathi ni vyema kupanga mapema juu ya usimamizi au mgawanyo wa mali zako kabla ya kifo.

Hitimisho

Ndugu msomaji hakuna mbadala wa ufahamu wako juu ya masuala ya mirathi, kwani utake usitake ni lazima yatakukuta iwe kwako au kwa ndugu yako wa karibu. Sote tu mashuhuda au tumehusishwa kwa njia moja ama nyingine katika migogoro ya mirathi. Ufahamu wetu juu ya habari hizi hautoshi na hauwezi kutusaidia isipokuwa tumechukua hatua stahiki na mapema, kwa kuwaona wataalam wa sheria waweze kukupa ushauri madhubuti namna ya kujiandaa na kuacha usimamizi salama wa mali zako na kutambua warithi wako halali.

Njia pekee ya kukusaidia au kumsadia mtu wa karibu yako ni kuandaa wosia yaani tamko la maandishi juu ya mali zako namna ambayo ungependa zitumike au kutunzwa endapo utafariki leo. Chukua hatua sasa.

‘Andika wosia sasa, maadam unaishi leo’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili